​SIMU, RESIPE YA ULAZAJI DAMU

Bottomline: Simu ni resipe ya uvivu unaomfanya mtu kutelekeza majukumu yake na kusababisha hasara kwake na wanaomzunguka

By Ramadhan O. Sigomba

“Dunia ina mambo, mambo na vijimambo.” Tukio hili nalikumbuka vyema kama yaumu yangu ya kuzaliwa. 

Ni juzi tu, siku ya kuadhimisha uhuru wa uanahabari kote duniani, tulipokuwa tukitoka mjini Eldoret kikazi, tukielekea kwenye studio. Gari lilibinganya masafa kwa mwendo wa wastani huku mpiga picha akibarizi kwenye kiti cha nyuma na tuliosalia tukipiga gumzo ili kumchangamsha dereva asipate lepe la usingizi na kubadilisha mkondo wa masimulizi haya. Hatua chache kabla ya kufika eneo la Kesses, tuliona  ng’ombe akila majani ya mahindi kwenye shamba la mwenyewe. Mchungaji alikua rijali wa umri wa makamu na hakuweza kumwona ng’ombe aliyekuwa akivamia mahindi kwenye shamba lingine kwani alikuwa ametekwa na kifaa cha mawasiliano kwa jina la SIMU iliyomfanya kuzama kwenye bahari ya luja na kuhatarisha shamba la mkulima aliyebidiika mithili ya mchwa ili kutatua maafa ya  ukame wa Januari. 

Ilimghairi dereva kusimamisha gari na kumkumbusha mchungaji yule majukumu yake na hatimaye alimfurusha ng’ombe kutoka shambani. Laiti dereva angepita kama upepo bila ya kusimama, huenda mkulima wa shamba lile angeathirika kwa kukosa mazao mbeleni. Hapo ndipo nilipotanabahi kwamba, simu ni resipe ya uvivu unaomfanya mtu kutelekeza majukumu yake na kusababisha hasara kwake na wanaomzunguka.

Lengo kuu la kubuniwa kwa rununu ni kurahisisha mawasiliano. Minghairi ya hilo, simu sasa imelemeza akili za wengi kupitia mitandao ya kijamii kama Facebook, Whatsapp na Twitter. Si vibaya kujihusisha na mitandao ya kijamii ila unapswa kutenga wakati maalum wa kuingia kwenye mitandao hiyo.   Ni jambo la kushangaza kuona mtu anaamkia facebook, kushinda whatsapp na kulala “mida ya wanga” kanakwamba ameajiriwa na mitandao hiyo ya kijamii. Sio chuku kulonga ya kwamba watu wengi wamekuwa watumwa wa simu kiasi cha kutelekeza majukumu yao. 

Wanafunzi hawana muda wa kudurusu mabuku yao kwasababu ya simu, hatimaye huishia kufeli. Baadhi ya  ajali zinazotokea barabarani husababishwa na madereva wanaotumia simu wanapopeleka gari. Wakati mwengine vyakula huteketea jikoni kwasababu mpishi ametekwa na simu. Simu imelemaza akili za wengi kwa kiasi cha kwamba, hawawezi kufikiria zaidi ya upeo wa simu. Kefule! Hata msalani hakuendeki bila ya simu.

Neno…  Unapotumia simu, tumia ikusaidie sio ikupotoshe. Yapo majukumu yenye umuhimu  na ya kupewa kipaumbele kushinda simu. Wenye masikio, wamesikia. Na wenye mashikio, shikilieni papo hapo. Wikendi njema.

Mwandishi: Ramadhan O. Sigomba

Barua Pepe: omarramadhan163@gmail.com

Twitter: @RamadhanOmar17

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s