SIASA HASI ZA KENYA


Wanaolonga hulonga, kadiri wanaosema wasemavyo  hadi ya kusema. Huu ndio mkondo unaofuatwa na siasa za taifa letu ambalo ni changa kisiasa. Hapa Kenya, aliye juu siku zote mfuate juu, kwani kushuka kwake chini ni dhambi isiyo na msamaha duniani wala ahera.

Siasa zetu si mbaya, na hakuna aliyependekeza na kunena siasa zetu ni dhaifu. Siasa zetu ni nzuri ila wanasiasa ndio wanaotanguliza matakwa yao. Wakiwa na malengo ya kujinufaisha wao wenyewe na aila zao. Wameuviringa aidha kuuvuruga mchezo wa siasa uwe mithili ya mtoto kinda anavyochezea tope.

Wanasiasa wetu wameufanya mchezo huu kuwa wenye uozo na mnuko mkuu sawia na mzoga  unavyokirihisha puani. Sisemi ni wanasiasa wote, bali tu ni wengi wanaodhihirisha paruwanja ya ukosefu wa ukomavu wao kisiasa.  Wengine ni wazuri ila Mungu akikupa kilema, hukukoseshi mwendo.

Cha kustaajabisha na kinachoudhi hasa ni kughafilika kwa wananchi wetu. Raia hawakanyiki. Matukio ya mitafaruku na vita ni vitu ambavyo vimetokea si kitambo ila wananchi hawakai kukumbuka asilani, sijui sababu na kigezo haswa, ama sijui ichukuliwe kwamba sikio la kufa halisikii dawa. 

Katika uchaguzi wa Agosti nane, watakaogombea nyadhifa mbalimbali na kuwakilisha vyama vyao,tumeshuhudia kisa kingine cha kudhihirisha dhahiri shahiri kwamba tungali mbali kuufikia ukomavu wa kisiasa. 

Wanasiasa hutulaghai. Kinaya ni kuwa , hatuoni tunavyopakwa mafuta kwa mgongo wa chupa katika kila uchaguzi. Wanatuletea sera zinazokaa nzuri machoni ila ni sera na ahadi za mdomo, katu zisiweze kutimizwa asilani.  Kama sera hizi zingekuwa sera hai, basi kufikia sasa naona  tungekuwa kama Marekani.

Mimi ni mmoja wa vijana ambao ni kioo cha jamii. Sisi ndisi tutakaobadilisha mambo.  Ninapotulia tuli, maji ya mtungi kando; mimi huwaza na kuwazua na kuchambua maswala ainati aidha tolatola chambilecho galacha wa muziki Saida Karoli,’’ Kweli nina hasara ipi nisipopiga kura.’’

Sitopenda hali ambapo kura zetu zinatufunga. Kura zetu zinaanzisha uhasama baina yetu. Kura zetu zinaleta vita dhidi ya ndugu wa nchi moja. Kura zetu zinasababisha maafa.

Tunawaabudu sana wanasiasa wetu. Aliyesema Raila ni Mungu ni nani? Ningependa kuonyeshwa sawia na aliyesema Uhuru ni Yesu kristo. Watu hawa hawaingii uongozini kuangalia mahitaji yetu, kwani ni Mungu pekee anayetupa mkate wa kila siku, nayo jitihada ya mja haiondoi kudura ya Mwenyezi Mungu.

Wanasiasa waovu wanatushawishi tuchukue sime, panga na shoka, tuanze kukabiliana mkabala; ndugu kwa ndugu, dada kwa dada. Kinaya ni kuwa wapiganapo wananchi, wanasiasa hawa wana usalama kwenye majumba yao maddal basari. Wako chini ya ulinzi mkali, sijaona mwanasiasa akichukua sime na kujitosa ukimbini tayari kukabiliana na raia. Umeona wewe?

Ashakum si matusi. Huu ni ubaradhuli wa hali ya juu mno. Mja wehedi anapofanya wananchi takriban millioni thelathini ushei kuzozana, inadhihirisha wazi jinsi tulivyo nyuma sana na mbali sana kuufikia ukomavu wa kisiasa. Turuhusu amani ienee miongoni mwetu. Letu ni kupiga kura na kurudi majumbani na kuyangoja matokeo. Matokeo huenda yakawa hasi, ama chanya vilevile. Hizi ni hali mbili ambazo lazima tujifunge nira kuona kwamba tuna ustahimilivu wa kuzikubali zote jinsi zijavyo. Ama kwa kulonga mithaki, wahenga  hawakutupwayapwaya kwa mipwaya ya kugwaya na kutuvika joho lisilo makamo yetu waliponena na kudhukuri kuwa; asiyekubali kushindwa si mshindani.

Tuwe na umoja na tucheze siasa safi. Siasa zilizokomaa. Kiongozi asitufanye tutengane. Matakwa yake ni tofauti sana na yetu. Sisi tunataka kuishi tu. Yeye anataka kuishi hadi ya maisha ya binadamu razini. Hivyo basi hatuko sawa asilani.
Luiz quincy thuo @ facebook

kunquincy254@gmail.com

quincythuo.wordpress.com

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s